Wadau wa maji Maswa wajadili uboreshaji wa huduma ya maji vijijini
24 June 2024, 1:07 pm
Serikali imeleta fedha nyingi za miradi ya maji vijijini lakini mwitikio wa wananchi kutumia maji ya bomba ambayo ni safi na salama ni mdogo sana na badala yake wanatumia maji ya madimbwi ambayo siyo safi na salama hali inayopelekea kuwavunja moyo wanaoleta fedha hizo.
Wadau wa maji wilayani Maswa mkoa wa Simiyu wamejadili namna ya uboreshaji wa huduma ya maji vijjijini chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini –RUWASA
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe, Aswege Kaminyoge amesema kuwa derikali imetenga fedha kwa ajili ya vijiji ambavyo vina changamoto ya maji ili navyo vipate maji.
Mhe Kaminyoge amesema serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya maji hivyo inategemea kuona matokeo ya mabadiliko katika huduma ya maji huku akiwapongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini – RUWASA Wilaya ya Maswa kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuleta huduma ya maji.
Meneja RUWASA Wilaya ya Maswa Mhandisi Lucas Madaha amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha ipo miradi wanayoendelea kuikamilisha ili kuhakikisha wanatekeleza kampeni ya kumtua mama ndoo kichwa.
Aidha Mhandisi Madaha amesema kuwa kwa mwaka ujao RUWASA Wilaya ya Maswa imejipanga kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji na kukamilisha miradi ambayo haijakamilika kwa mwaka unaoisha.
Kwa uapande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Ruwasa Willison Magaigwa amesema kuwa licha ya Serikali kupeleka miradi ya Maji bado mwitikio ni Mdogo wa Wananchi kutumia Maji ya Bomba ambayo ni Safi na Salama
Baadhi ya Madiwani waliohudhuria Kikao hicho cha Wadau wa Maji wamehoji kuwa ni vigezo gani vinavyotumika kubaini changamoto za Maji kwenye Vijiji na watu gani wanaowashirikisha katika kubaini changamoto hizo.