RC Nawanda aagiza halmashauri kutenga bajeti ya michezo mashuleni
31 May 2024, 7:16 pm
Utengaji wa bajeti ya ununuzi wa vifaa vya michezo mashuleni utaongeza wanamichezo hivyo kutengeneza ajira nyingi na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Na.Daniel Manyanga
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya Nawanda ameziagiza halmashauri zote mkoani hapo kutenga fedha za ununuzi wa vifaa vya michezo mashuleni na uendeshaji wa michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Maswa , Aswege Kaminyoge aliyekuwa akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya Nawanda kwenye ufunguzi wa michezo ya wanafunzi wa shule za msingi ngazi ya mkoa UMITASHUMTA katika shule ya sekondari ya wasichana ya Maswa girls.
Aswege Kaminyoge amesema kuwa michezo ni ajira ambayo inalipa pesa nyingi hivyo halmashauri zitengeneze mazingira mazuri kwa wanamichezo ili kuweza kukuza vipaji vyao kuanzia mashuleni hadi kitaifa kwa kutenga bajeti ya ununuzi wa vifaa vya michezo pamoja uendeshaji wa michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA kitaifa.
Aswege Kaminyoge amewataka wanamichezo watakaochaguliwa kwenye timu ya mkoa itakayoenda kuwakilisha kitaifa mkoani Tabora kuwa na nidhamu wawapo kambini na kule mkoani Tabora pamoja na kujituma wakati wote wa mashindano huku maafisa elimu,michezo na utamaduni wakitakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kujenga uelewa wa michezo mashuleni.
Awali mwakilishi wa afisa elimu mkoa wa Simiyu,Mwl Esther Marwa ametaja michezo watakayoshiriki hivyo amewaomba wanafunzi waliochaguliwa kambini kuwa na nidhamu na kudumisha usafi wakati wote wa michezo.