Ongezeko la mamba mto Simiyu latishia maisha ya wananchi
11 March 2024, 5:43 pm
Na,Alex Sayi-Simiyu
Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania TAWA Kanda ya Ziwa, wabainisha kuwa uwepo wa mtawanyiko wa Maji kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha kwa hivi sasa kumechangia ongezeko la Mamba mto Simiyu hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi wanaoishi karibu na mto huo.
Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA)Kanda ya Ziwa wametahadharisha wakazi waishio pembezoni mwa Mto Simiyu juu ya uwepo wa ongezeko la Mamba kutokana na Mvua nyingi zinazoendelea kunyesha kwa hivi sasa.
Akizungumza na Sibuka Fm Redio, Lusato Masinde Afisa Wanyamapori kitengo cha ujirani mwema TAWA Kanda ya Ziwa amesema kuwa kumekuwa na matukio ya watu kujeruhiwa au kuliwa na Mamba kutoka na ongezeko la Mamba Mto Simiyu
Masinde ameongeza kuwa hivi karibuni kumekuwa na matukio ya vifo vitokanavyo na Mamba Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu na Bunda Mkoani Mara na kuwataka wazazi kuchukua tahadhari kwa watoto wao.
Innocent Kavela Kaimu mtendaji Kijiji cha Ipililo Kata ya Ipililo Wilayani Maswa Mkoani hapa amezungumzia tukio la mtoto mwenye umri wa miaka (9)Masanja Maduhu kujeruhiwa na Mamba hali iliyopelekea kifo chake.
Aidha kwa upande wake Mwl Meckiad Ruyingo makamu Mkuu Shule ya Sec Bushashi amesema kuwa anaishukuru (TAWA)kwa kufika Shuleni hapo nakutoa Elimu ya kuchukua tahadhari dhidi ya mnyama huyo.
Mariam Salumu na Dotto Mashosho wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bushashi wameishukuru TAWA kwa elimu walioipata hali ambayo itawasaidia kuchukua tahadhari dhidi ya mnyama Mamba.