Red Cross: Mwanamke ni nguzo muhimu kwa taifa
10 March 2024, 8:38 am
Chama cha msalaba mwekundu mkoani Simiyu kimesherekea siku ya Wanawake duniani kwa kufanya usafi katika hospitali ya wilaya ya Maswa katika kutambua na kuthamini mchango wa Wanawake katika Nyanja mbalimbali za kimaendeleo nchini.
Na,Paul Yohana
Katika kuenzi na kuthamini mchango wa Wanawake kwenye ujenzi nchi duniani kote Chama cha Msalaba mwekundu Mkoa wa Simiyu kimesherekea siku ya wanawake duniani kwa kufanya usafi katika hosptal ya wilaya ya Maswa ili kuongeza chachu na hamasa kwa wananchi na wanachama wengine hasa wanawake kujiunga na chama hicho
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa msalaba mwekundu mwenyekiti wa chama hicho kutoka Kikundi Cha Upendo,Bi.Ester Lukas amewaomba wanachama hao kuwa na moyo wa kujitolea katika kuenzi siku ya Wanawake duniani ambayo hufanyika kila mwaka mnamo tarehe 08.march ili kutambua mchango wa Wanawake katika Nyanja mbalimbali.
Aidha Afisa Afya wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa Bi, Asha Muharam ameupongeza umoja wa wanachama hao kwa kujitoa kwao kwenye jamii hasa kwa kufanya usafi katika eneo la hospitali.
Dkt.Boniphace Mabonesho ni Afisa Afya na mafunzo toka msalaba mwekundu amesema kuwa chama hicho kimeamua kusherehekea siku ya Wanawake dunia kwa kufanya usafi katika eneo la Hospitali ya wilaya ikiwa ni moja wapo katika kuenzi na kuthamini harakati za wanawake.
Joseph Magembe ni mmoja wa wanachama amewaomba wananchi ushirikiano wao na kuwaunga mkono katika kuboresha chama hicho.