Takukuru Simiyu yaokoa zaidi ya shilingi milioni 70
25 February 2024, 6:29 pm
Na Nicholaus Machunda
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa wa Simiyu imefanikiwa kuokoa fedha zaidi ya shilingi milioni sabini zilizotaka kufanyiwa ubadhirifu katika Chuo cha Maafisa Tabibu wilayani Maswa.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Naibu Mkuu wa Takukuru mkoani hapa Aron Misanga amesema kuwa fedha hizo zilipelekwa chuoni hapo kwa ajili ya posho ya kazi maalum iliyofanyika lakini Takukuru ilipofuatilia ilibaini kuwa wahusika hawakupewa fedha zao.
Aidha Naibu Mkuu wa Takukuru amesema kuwa wamefanya ufuatiliaji katika ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa POS katika halmashauri ya Maswa pamoja na ununuzi wa pamba kupitia Amcos ya mbalimbali mkoani hapa na kugundua ubadhirifu mkubwa uliokuwa umefanyika.
Katika uchambuzi wa mfumo Takukuru mkoa wa Simiyu ilibaini mapungufu makubwa katika utoaji wa huduma katika Idara ya Ardhi hali inayopelekea kuwepo kwa mianya ya rushwa.
Takukuru mkoa wa Simiyu inatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na utoaji wa taarifa za rushwa na ubadhirifu wa fedha za miradi inayoendelea kujengwa.