Zaidi ya watoto laki moja kupata chanjo ya surua, rubela Maswa
8 February 2024, 8:50 pm
Watoto wenye umri wa kuanzia miezi tisa hadi chini ya miezi hamsini na tisa kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa Surua na Rubela katika kampeni ya kitaifa ya siku nne.
Na,Daniel Manyanga
Zaidi ya Watoto Laki Moja walio na umri chini ya Miaka mitano (Chini ya Miezi 59 ) Wilayani Maswa mkoani Simiyu wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya Ugonjwa wa Surua na Rubela katika kampeni ya Kitaifa ya Siku Nne.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Chanjo wilaya ya Maswa Ndg.Abel Machibya Mapema Leo hii wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake .
Machibya amesema kuwa mpango wa halmashauri hiyo ni kuwafikia Watoto Laki Moja na kumi elfu mianane tisini na moja (110891) kwa kipindi Cha siku Nne kuanzia tarehe 15 Hadi 18 ya mwezi huu katika sehemu zilizotengwa kwa ajili ya zoezi hilo.
Machibya ameongeza kuwa chanjo ya Surua na Rubela hutolewa kwa Watoto wenye umri wa kuanzia miezi 9 Hadi chini ya miezi 59 (Chini ya Miaka 5) ikiwa na lengo la kuwakinga Watoto na ugonjwa huo pamoja na kuongeza Kinga kwa walengwa.
Katika hatua nyingine Abel Machibya amewaomba Wazazi na Walezi walio na Watoto wenye miaka chini ya mitano kuwapeleka katika vituo tajwa Ili waweze Kupata chanjo ya Surua na Rubela lengo ni kuwakinga na ugonjwa huo ambao ni hatari Sana kwa Watoto.