Wadau wa afya waombwa kujitokeza kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kulelea watoto njiti ili kupunguza vifo vya watoto wilayani Maswa.
28 February 2022, 3:45 pm
Taasisi na wadau mbalimbali wa afya wameombwa kujitokeza kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kulelea watoto njiti katika hospitali ya wilaya ya Maswa ili kupunguza vifo vya Watoto na kuiongezea hospitali hiyo uwezo wa kuwahudumia watoto wengi wanaohitaji huduma hiyo kwa wakati mmoja.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dk. Bwire James Robert amesema kuwa kwa sasa wanao uwezo wa kuwahudumia watoto 10 kwa wakati mmoja, kutokana na msaada wa vifaa uliotolewa na taasisis isiyokuwa ya kiserikali ya Dorice Mollel Foundation.
Aidha Dk Bwire amesema kuwa huku uhitaji wa vifaa hivyo hospitalini hapo bado ni mkubwa, hivyo kuwaomba wadau mbalimbali wa afya kuendelea kujitokeza na kusaidia upatikanaji wa vifaa hivyo kwa ajili ya watoto njiti.
Dk Bwire amevitaja vifaa ambavyo wamevipata kwa msaada wa Dorice Mollel Foundation na kusema kuwa vimesaidia kwa kiasi kikubwa utolewaji wa huduma kwa watoto njiti na kwamba tangu vifaa hivyo wiwasili hospitalini hapo vimesaidia kuepuka vifo kwa watoto Njiti na hawajatoa rufaa kwa watoto kwenda kutibiwa Bugando..
Kwa upande wake Dorice Mollel ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya Dorice Mollel Foundation ameeleza kuwa kilichowasukuma kutoa msaada wa vifaa hivyo ni kutokana na changamoto ya matibabu kwa watoto njiti hali iliyokuwa inapelekea wengi kupoteza Maisha kwa kukosa huduma hiyo.
Kwa mujibu wa mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Maswa Dk. Bwire James Robert amesema kwa sasa wanapokea watoto njiti 16 – 23 kwa mwezi, kutoka wilayani humo na maeneo mengine ya jirani na wilaya hiyo..