Rais atoa zana za kilimo Maswa kuongeza uzalishaji wa pamba
13 March 2024, 10:44 am
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mh Aswege Kaminyoge amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zana za kilimo kwa wakulima wa kata ya Senani ili kumsaidia mkulima katika kuongeza tija katika zao la pamba.
DC Kaminyoge ametoa shukrani hizo wakati wa kuzindua zana hizo za kilimo katika kata ya Senani na kuwataka wakulima kuongeza uzalishaji ili kurudisha fadhira kwa Rais aliyetoa zana hizo.
Kaminyoge amewataka wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo ili kuongeza tija ya uzalishaji wa zao la pamba na kuweza kujikwamua kiuchumi huku akiwataka viongozi waliokabidhiwa kusimamia ugawaji wa zana hizo bila upendeleo.
Ally Mabrouk ni mwakilishi wa Bodi ya Pamba wilayani Maswa amesema zana hizo za kilimo ni kwa ajili ya wakulima kuwasaidia na vitatumika bure hivyo mkulima atahitaji kwenda kujiandikisha, kukopeshwa na kwenda kutumia kisha kurudisha.
Akijibu swali la Jilala Ngasa mkulima wa kata ya Senani kuhusu upimaji wa udongo upi unafaa kwa kilimo, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Robert Urassa amesema vifaa vya kupimia udongo tayari vimewasili na muda wowote zoezi litaanza mara moja na wakulima watapimiwa udongo na kupata majibu pamoja na kupewa ushauri.
Baadhi ya wakulima wa kata ya Senani ambapo mradi huo wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT ) wamemshukuru Rais kwa kuwaletea vifaa hivyo vya kilimo kwani vitasaidia kuongeza uzalishaji wa tija katika zao la pamba.