Migogoro ya ardhi, mirathi yapatiwa mwarobaini Maswa
27 January 2024, 7:29 pm
“Wananchi waitumie wiki na siku ya sheria kupata elimu ya kisheria ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima hasa migogoro ya ardhi na mirathi kwa sasa hairipotowi kwa wingi katika vyombo vya kutoa haki.”
Na,Daniel Manyanga
Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Mhe,Aswege Kaminyoge amewaomba Wananchi wilayani hapo kuitumia wiki na siku ya sheria kupata elimu ya maswala ya kisheria ili kumaliza migogoro ya ardhi na mirathi ambayo imeonekana kuwa mingi na kutishia amani kwa baadhi ya jamii.
Kaminyoge ametoa rai hiyo mapema leo hii akiwa katika viwanja vya stund ya zamani wakati wa ufunguzi wa wiki ya sheria ambapo amesema kuwa migogoro mingi inayoonekana kuripotiwa mara kwa mara kwenye vyombo vya kutoa haki ni mogogoro ya ardhi na mirathi hivyo ni vyema sasa Wananchi kuitumia wiki hiyo kuelimishwa na hatimaye kuondokana na migogoro hiyo isiyo ya lazima.
Kaminyoge ameongeza kuwa kuna migogoro mingine midogo midogo haipaswi hata kuripotiwa katika vyombo vya kisheria endapo wananchi wataitumia wiki ya sheria kupata elimu ya masuala ya kisheria ambayo itasaidikia kupunguza au kumaliza migogoro baadhi ambayo haihitaji usaidizi wa mahakama.
Awali hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Maswa Mhe,Enos Missana amesema kuwa maadhimisho ya wiki ya sheria hutumika kama jukwaa maalumu linalowakutanisha Mahakama na wadau wake muhimu ili kutoa elimu ya shughuli zitolewazo na mahakama na wadau wake walio katika munyororo wa utoaji haki.
Katika hatua nyingine Kaminyoge amemuagiza Katibu tawala wilaya na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri wa wilaya ya maswa kuhakikisha wanashirikiana na Mahakama ya wilaya hiyo kuendelea kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa wiki ya sheria ili waweze kujitokeza kwa wingi siku ya kilele hicho pamoja na wakuu wa idara mbalimbali kuweza kuhudhuria siku hiyo.
Uzinduzi wa wiki ya sheria umeenda sambamba na kaulimbiu isemayo ‘’Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa taifa Nafasi ya Mahakama na Wadau katika kuboresha mfumo Jumuishi wa haki Jinai”