Maafisa tarafa, VEO na WEO kusimamia uandikishaji wa wanafunzi Maswa
18 December 2023, 9:40 am
Zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wanaoanza masomo katika mwaka masomo 2024 kwa elimu ya msingi na sekondari lipo chini ya afisa tarafa, watendaji wa kata na vijiji kwa kushirikiana kwa ukaribu na wenyeviti wa vijiji na vitongoji.
Na Daniel Manyanga
Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Mhe.Aswege Kaminyoge amewataka Maafisa Tarafa,Watendaji wa kata na Vijini kuhakikisha wanasimamia ipasavyo zoezi la uandikishaji kwa Wanafunzi wa awali na msingi pamoja kidato cha kwanza katika mwaka wa masomo 2024 masomo yatakayoanza mwezi January.
Kaminyoge ametoa Rai hiyo wakati akitoa salamu za kheri ya Krismas na mwaka mpya kwa Wafanyakazi na Wananchi wilayani hapo katika mkutano wa Mwaka wa Wadau wa Sekta ya Maji ulioandaliwa na wakala wa Maji na usafi wa mazingira Vijijini Wilayani hapo (RUWASA) uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya hiyo.
Kaminyoge amesema kuwa tunaelekea mwaka 2024 ambapo kunazoezi la kuandisha Wanafunzi watakao anza elimu ya msingi na awali lakini pia elimu ya sekondari kwa wanafunzi ambao wamemaliza elimu ya msingi ambapo wanatakiwa kuanza masomo mara moja pasina kuwa na kisingizio chochote kutokana na serikali ya awamu sita ya rais Mhe.Dr.Samia Suluhu Hassan kutoa elimu bila malipo.
Kaminyoge ameongeza kuwa swala la uandikishaji siyo swala la Mkuu wa Shule,Mwalimu Mkuu na wala Mkuu wa wilaya badala yake swala la kuhakikisha wanafunzi wanaandikishwa na kuanza masomo yao Msingi na Sekondari ni jukumu la Afisa Tarafa,Watendaji wa Kata na Vijiji wakishirikiana kwa ukaribu na Wenyeviti wa Kijiji na Kitongoji .
Katika hatua nyingine Mhe.Aswege Kaminyoge amemuomba mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,Maisha Mpita kukaa na Madiwani ili waweze kuona namna nzuri ya kuwashirikisha wananchi kuweza kuchangia ujenzi wa miundombinu muhimu ya vyoo licha ya serikali ya awamu ya sita kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa vyoo katika baadhi ya shule za msingi na sekondari ambazo zinaupungufu wa matundu ya vyoo.