RUWASA yakabiliwa na uhaba wa vitendea kazi, wataalam
19 November 2023, 4:58 pm
(RUWASA) ndani ya miaka miwili ya utawala wa awamu ya sita wa Rais Samia Suluhu imefanikiwa kutoa huduma ya maji vijijini kwa asilimia 74.
Na Alex Sayi
Wakala wa Maji Safi na Mazingira Vijijini wilayani Maswa mkoani Simiyu RUWASA umebainisha kuwa unakabiliwa na ufinyu wa vitendea kazi vya kutosha ikiwemo ufinyu wa bajeti, magari na rasilimali watu.
Hayo yamebainishwa na meneja wa mamlaka hiyo wilaya hapa Mhandisi Lukas Madaha wakati akitolea taarifa ya utekelezaji wa wakala huyo mbele ya madiwani kwenye baraza lililoketi Novemba 07 mwaka huu kwenye ukumbi wa halmashauri.
Mhandisi Madaha amesema kuwa hali ya upatikanaji wa maji kwa miaka miwili sasa wilayani Maswa umefikia 74% kutoka 68% za awali, kufuatia serikali ya awamu ya sita kumwaga fedha nyinga kwa (RUWASA).
Sanjari na hayo baadhi ya madiwani waliendelea kuhoji juu ya utendaji kazi wa wakala huyo kwa kushindwa kutoa huduma ya maji kwa baadhi ya kata, Sadick Duttu Diwani wa kata ya Senani alitaka kujua lini kituo cha afya Senani kitapata huduma hiyo ya maji.
Diwani wa kata ya Mwandete Juliana John amesema kuwa wananchi wa kata hiyo kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na adha ya upatikanaji wa maji hasa wakati wa kiangazi hali inayopelekea wananchi wa kata hiyo kununua maji dumu moja kwa shilingi elfu moja na mia moja.
Diwani wa kata ya Budekwa wilayani hapa Esther Ng’holongo amesema kuwa hali ya upatikanaji wa maji katani hapo ni mbaya kwa kuwa wananchi wanalazimika kutumia hadi siku mbili kupata maji yanayopatikana mtoni.