Sibuka FM

Maswa: Vikundi 82 kufikishwa mahakamani kwa kushindwa kurejesha mikopo.

13 April 2023, 4:44 pm

NA,ALEX.F. SAYI

Vikundi 82 vya Wanawake,Vijana na Walemavu vimeendelea kufikishwa Mahakamani na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa kushindwa kurejesha zaidi ya Sh.Mil,129.9 walizokopeshwa na Halmashauri hiyo kwa  mwaka wa fedha 2021/2022

Akizungumza na Sibuka Fm, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Maswa na Diwani wa Kata ya Shanwa Paul Maige, amesema kuwa Baraza la madiwani lilishaelekeza kufikishwa Mahakamani vikundi vyote vilivyoshindwa kurejesha mikopo hiyo.

Maige ameongeza kuwa Baraza hilo linaamini kuwa Ofisi ya  Afisa maendeleo na Afisa mikopo wanashughulikia suala hilo kwa kuwa Bajeti ya 10% inayotengwa na Halmashauri kila mwaka haitoshelezi kuvikopesha vikundi vyote, hivyo marejesho ya mikopo hiyo itasaidi vikundi vingine kukopeshwa.

“Tunajitaidi kuongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili tuweze kutenga kiasi kikubwa kuweza kuvikopesha vikundi vinavyoomba ila kwa sasa tunachangamoto ya Bajeti ingawa tunaongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani.”Amesema Mwenyekiti

Akizungumzia suala la ukusanyaji wa Mapato Mwenyekiti huyo amesema kuwa wanatarajia kukusanya zaidi ya Sh.Bil,4 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ikilinganishwa na makadirio ya Bajeti ya Sh.Bil 2.2 kwa mwaka wa fedha  uliopita 2021/2022 na tayari hadi sasa wameshakusanya nusu ya  mapato hayo.

Akizungumzia suala hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Walaya  hiyo ,Simon Berege amesema kuwa mashauri  ya vikundi 50 yamefikishwa Mahakamani kati ya  vikundi 82 na  tayari zaidi ya Sh.Mil 98.4 zimeshalipwa na vikundi vingine vikiendelea kulipa kwa hiali mikopo hiyo kwa kuhofia kufikishwa Mahakamani.

“Pamoja na fedha hizi kurejeshwa bado tunauhaba wa Bajeti hata hivyo bado tunaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani  na kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 tumetenga zaidi ya Sh.Mil 300 kwa ajili  ya makundi ya Wanawake,Vijana na Walemavu.”Amesema Mkurugenzi.

Aidha kwa upande wake Mkuu wa Divisioni ya Maendeleo ya Jamii Wilayani hapa Roghers Lyimo amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 zaidi ya Sh.Mil 200  zilikopeshwa kwa vikundi 25 kati ya vikundi 80  vilivyoomba mkopo.

“kwa mwaka wa fedha 2021/2022 tulikopesha zaidi ya Sh.Mill 200 na kwa mwaka huu wa fedha robo ya kwanza Julai na Machi 2022/2023 tumekopesha vikundi 47 kati ya vikundi 152 vilivyoomba zaidi ya Sh.Mil 700 kati ya Sh.Mil 300 zilizotengwa,hivyo bado tunakabiliwa na uhaba wa Bajeti kuweza kuvikopesha vikundi vinavyoomba mikopo;”Amesema Lyimo.