Ubovu wa barabara wachangia kushuka kwa mapato Makete
February 15, 2024, 7:34 pm
Ubovu wa barabara Makete umepelekea kupotea kwa mapato hali iliyomfanya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Mh. Christopher Fungo kuagiza mamlaka husika kuchukua hatua za maksudi ili kunusuru kupotea kwa mapato .
Na Ombeni Mgongolwa
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Makete, leo Februali 15, 2024, limekaa kikao cha robo ya pili cha kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata 23 zilizopo katika halmashauri ikiwa ni mwaka wa fedha wa 2023-2024.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Mhe. Christopher Fungo, amesema kuwa lengo la kikao ni kujadili taarifa za maendeleo ya miradi, na kwamba changamoto kubwa ya ubovu wa barabara ndani ya kata hizo zimepelekwa kwa mamlaka husika ambao ni TARURA ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Ndg. William M. Makufwe, amesema kuwa mpango wa Halmashauri ni kuhakikisha zile barabara muhimu zote zinaingizwa TANROAD, ili ziweze kutengewa bajeti kubwa ambayo itarahihisha usafiri pamoja na ukusanyaji wa mapato, tofauti na bajeti za TARURA.
Sambamba na hayo, Ndg. Makufwe, amesema kuwa, kutofanyika kwa vikao vya kisheria katika mji mdogo wa Iwawa uliopo halmashauri ya Wilaya ya Makete, ni kutokana na ufinyu wa mapato katika halmashauri hiyo sambamba na muingiliano wa majukumu yaliyo nje ya bajeti na kupelekea kupungua kwa mapato.
Nao baadhi ya Madiwani, wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, wameiomba TARURA, kuhakikisha kuwa wanaboresha barabara zote zilizopo katika halmashauri hiyo ili mapato yaweze kupatikana, na kuboresha huduma za wananchi katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na kuziomba baadhi ya barabara kuingia kwenye mamlaka za TANROAD.
Ikumbukwe kuwa, kikao cha Baraza la Madiwani, cha kupitia na Kujadili taarifa za Miradi ya Maendeleo ya Kata, hufanyika kila baada ya robo kukamilika, ili kujadili namna Bora ya Utekelezaji wa Miradi hiyo.