Kitulo FM
Kitulo FM
March 17, 2026, 5:20 pm

Kutokana na wimbi la wizi katika maeneo mbali mbali jamii imetakiwa kuacha vitendo hivyo na badala yake wajike katika shughuli halali za kujipatia kipato
na mwandishi wetu.
Mahakama ya Wilaya ya Makete Mkoani Njombe imemuhukumu Anyowise Gehezi sanga maarufu kwa jina la Paulo mkazi wa tandala kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani kwa kosa la kula njama kutenda kosa pamoja na kifungo cha miaka minne kwa kosa la pili la wizi wa pikipiki.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa mnamo tarehe 22/2/2026 mshtakiwa huyo pamoja na wengine watatu akiwemo sauti fillimon mbilinyi, Nigeria godeni mbilinyi pamoja na clemence malyo maarufu kwa jina la swalo wote wakazi wa tandala walitenda makosa hayo mawili ya kula njama kutenda kosa pamoja na wizi wa pikipiki yenye usajili namba MC 854 EUN mali halali ya Daren Hezeza Sanga
Hata hivyo Katika kosa la kwanza la kula njama kutenda kosa ni kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023 na katika kosa la pili la wizi ni kinyume na kifungu cha 258 (1) kikisomeka pamoja na kifungu namba 265 vifungu vyote vikiwa vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023
Aidha baada ya upelelezi wa makosa hayo kukamilika waliweza kupelekwa katika mahakama ya wilaya ya makete 5/3/2026 na kusomewa mashtaka mawili yanayowakabili na waliweza kukana kutenda makosa hayo
Hata hivyo mnamo tarehe 16/3/2026 shauri hilo la jinai lenye namba 4908/2026 lilikuja kwaajili ya kusikilizwa ambapo kabla ya shauri kuanza kusikilizwa washtakiwa wote wanne waliweza kukumbushwa mashtaka yao yanayowakabili ambapo mshtakiwa namba moja ambaye ni Anyowise Gehezi sanga maarufu kwa jina la Paulo aliweza kukiri kutenda makosa hayo
Kwa upande wa jamuhuri uliiomba mahakama iweze kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo
Mahakama ilizingatia maombi ya upande wa jamuhuri pamoja na maombolezo ya mshtakiwa namba moja ambaye ni Anyowise Gehezi sanga na kutoa uwamuzi wa mshtakiwa huyo kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani kwa kosa la kula njama kutenda kosa pamoja na kosa la pili la wizi wa pikipiki
Hata hivyo Imeelezwa mahakamani hapo kuwa shauri hilo litaendelea tena kesho kwa washtakiwa watatu ambao walikana kutenda makosa hayo
Hukumu hiyo dhidi ya mshtakiwa ilitolewa jana na hakimu mkazi mfawidhi mwandamizi mhe Ivarn Msack pamoja na mwendesha mashtaka wa serikali na mkaguzi wa polisi mhe Benstard Mwoshe