Kipagalo watakiwa kujitoa kwa moyo utekelezaji wa miradi
April 16, 2024, 9:46 am
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Mhe. Christopher Fungo, amewataka wakazi wa kata ya Kipagalo kujitoa kwa moyo katika ujenzi wa kituo cha Afya cha kata hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Mhe. Christopher Y. Fungo, leo Aprili 15, 2024, akiwa ameongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg. William M. Makufwe, wamefanya ziara katika Kata ya Kipagalo, ili kujionea maandalizi ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Kipagalo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Fungo, ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia fedha kwaajili ya ujenzi wa Kituo hicho cha Afya Kipagalo, ambacho kitajengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, TASAF.
Aidha, Mhe. Fungo, amewataka wananchi wa Kata hiyo, kujitoa Kwa moyo katika kuchangia nguvu kazi kulingana na miongozo ya TASAF inavyotaka, ili kuleta wepesi katika utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Ndge. William M. Makufwe, ameitaka, Kamati ya Usimamizi ngazi ya Jamii,(CMC), kushirikiana na uongozi wa kata na kijiji ili waweze kupanga ratiba ya kazi za utekelezaji wa mradi huo.
Sambamba na hayo, Ndg. Makufwe, ameiagiza, CMC, kuhakikisha kuwa, wanadhibiti upotevu wa vifaa vya ujenzi, kwa kuweka utaratibu mzuri wa usimamizi na ulinzi wa vifaa hivyo na kufuata maelekezo ya wataalam kutoka halmashauri.
Akizungumza kwa niaba ya Wananchi, Diwani wa Kata ya Kipagalo, Mhe. Nehemiah Kayanda Sanga, ameishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi huo ambao utakuwa mkombozi kwa wakazi wa Kata hiyo na Vijiji jirani.
Aidha, Mhe. Sanga ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, kwa kuitembelea Kata hiyo, ili kujionea maandalizi ya ujenzi wa Kituo hicho cha Afya cha Kata ya Kipagalo.
Ikumbukwe kuwa, mradi huo wa Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya cha Kata ya Kipagalo, utatumia kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 805, ikiwa ni Fedha kutoka TASAF.