Serikali yatoa fedha kujenga kituo cha afya Mfumbi Makete
February 8, 2024, 5:28 pm
Kata ya Mfumbi ni miongoni mwa kata ambazo zimepewa mradi wa ujenzi wa kituo cha afya ikiwa ni mpango wa halmashauri ya wilaya ya Makete kujenga vituo vya afya ktika kata zote ambazo hazina vituo vya afya pamoja na kuboresha miundombinu katika vituo vyenye uchakavu wa miundombinu.
Na Lulu Mbwaga
Mkuu wa Wilaya ya Makate, Mhe. Juma S. Sweda, ameipogeza Halmashauri ya Wilaya ya Makete, pamoja na kuishukuru Serikali ya Tanzania, kwa kutenga fedha ili kujenga kituo cha Afya Kata ya Mfumbi, kutokana na umuhimu wake katika jamii.
Akizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi wa Ujenzi huo, Mhe. Sweda, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imelenga kuboresha huduma za Afya, kwa Mama na mtoto kwa kuwa wamekuwa wakipoteza uhai wao hasa wakati wa kujifungua.
Kwa upande Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Ndg. William Makufwe, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila kata inakuwa na kituo cha Afya, na kwamba hadi sasa Serikali imeshajenga vituo vya Afya vitano, katika Kata za Halmashauri hiyo ambazo zimekuwa na uhitaji mkubwa kutokana na wingi wa watu pamoja na sababu za Kijiografia za upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Mhe. Hawa Kader, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajengea kituo hicho cha Afya bora kabisa, ambacho kitaenda kutatua kero ya mufa mrefu katika upande wa uzazi.
Baadhi ya akinamama wa Kijiji cha Kimani, wamemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajengea kituo hicho, kwakuwa ametatua changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwatesa kwa muda mrefu.
Ikumbukwe kuwa mradi huo wa kituo cha Afya cha Mfumbi, unajengwa kwa kutumia mapato ya ndani, kwa kushirikiana na TASAF, ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 264,553,226.74 zimetumika katika kuhakikisha kuwa majengo mawili ya OPD na Mama na Mtoto yanakamilika kwa wakati ifikapo mwezi wa nne 2024.