Zaidi ya miti 2,000 yapandwa Makete kutunza, kuhifadhi mazingira
January 22, 2024, 8:36 pm
katika kuendeleza juhudi za utunzaji wa mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Makete kupitia Idara ya Mazingira imeendelea kutoa elimu kwa jamii ikiwa nipamoja na kupanda miti zaidi ya Elufu mbili (2000) katika kata ya Tandala
na Aldo Sanga
Zoezi la upandaji Miti Kiwilaya limezinduliwa leo tarehe 22 Januari, 2023 katika shule ya Msingi Ikonda iliyopo Kata ya Tandala Wilayani Makete Mkoa wa Njombe.
Zoezi hilo limefanyika na Viongozi wa Serikali kwa kushirikiana na Wananchi wa Ikonda ambapo zaidi ya miti 2,000 imepandwa kwa lengo la kutunza na kuhifadhi mazingira.
Afisa Tarafa ya Lupalilo Ndg. Augustino Ngailo amezindua upandaji miti kiwilaya kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda ambapo amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Ikonda kwa kujitokeza kwa wingi katika kupanda miti hiyo
Ngailo amesema shughuli ya kupanda miti na kuitunza ni muhimu, kwani Wilaya ya Makete ni muhimili wa vyanzo vya maji hivyo ni jukumu lao kuitunza miti hiyo
Aidha ameongeza kuwa hivi karibuni kumetokea athari zilizosababishwa na mvua iliyoambatana na upepo kuleta madhara hivyo miti inasaidia kupunguza madhara yatokana na upepo mkali
Moses Ndiu Mhifadhi Misitu Wilaya kupitia Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) amewaasa wananchi kuitunza miti hiyo kwani wilaya ya Makete imekuwa ikipanda miti mara kwa mara lakini inayokua ni michache haioti kwa sababu haihudumiwi hivyo ni vema ikatunzwa ili kutunza mazingira na kuzuia maafa yatokanayo na mvua iliyoambatana na upepo
Ameongeza kua miti hii imetolewa na wakala wa huduma za misitu Tanzania bure na inagharimu Shilingi 200 kwa kila mche na kwa mkoa wa Njombe imepata Miche milioni moja na nusu ambayo ni zaidi ya thamani ya Milioni miatatu
Diwani wa kata ya Tandala Mhe. Daniel Hatanaka amesema ni jukumu lao kuitunza miti yote iliyopandwa na kila mwananchi anatakiwa kuitunza na kuwapa watoto elimu ya umuhimu wa miti
Halmashauri ya Wilaya ya Makete imekuwa ikotoa elimu ya kupanda na kutunza miti ili kutunza mazingira katika taasisi binafsi, Ofisi za Serikali na Wananchi huku bado ikikabiliwa na uharibifu wa mazingira kwa kuchoma moto hovyo huku zaidi ya hekari za miti 3,000 mwaka 2023 zimechomwa moto huku uchumi wengi wa wananchi wa Makete inategemea mazao ya misitu na kilimo