Waziri Bashungwa aagiza kasi zaidi ujenzi barabara ya Makete-Mbeya
January 22, 2024, 8:04 pm
Waziri Bashungwa amefanya ziara katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Mbeya- Makete kwa kiwango cha lami huku akitoa maelekezo kwa mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ikiwa nipamoja na kuongeza mitambo ili kuendana na mkataba wamradi huo
Na Aldo Sanga
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa ametoa muda wa wiki tatu kwa Mkandarasi wa kampuni ya China National Aero-Technology International Engineering Corporation (AVIC) anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete sehemu ya Kitulo – Iniho (km 36.3) kwa kiwango cha lami kufikisha vifaa na wataalamu wote katika eneo la mradi ili kazi ifanyike kwa haraka kwa mujibu wa mkataba
Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo leo Januari 22, 2024 akiwa Wilayani Makete Mkoani Njombe katika ziara ya kikazi na kukagua utekelezaji wa mradi huo ambao upo nyuma kwa mujibu wa mkataba
Kadhalika Bashungwa ameutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) kumsimamia Mkandarasi huyo kwa karibu na kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana.
Ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta Bilioni 82 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kutokana na umuhimu wa wananchi wa Wilaya ya Makete na Mkoa wa Njombe katika kuleta maendeleo na kuinua uchumi wa wananchi.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa amepokea maombi ya kuunganisha Wilaya ya Makete na Busokelo Mkoani Mbeya na tayari usanifu unakwenda kuanza kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe.
Kwa upande wa Mbunge wa Makete Mhe. Festo Sanga ameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwani ni kiungo muhimu kiuchumi kati ya mkoa wa Njombe na Mbeya
Akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Jephason Nko, ameeleza kuwa mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 4.2 ambapo unasimamiwa na Kitengo cha TECU kutoka wakala huo huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Julai 2026