Watumishi 5 wafukuzwa kazi halmashauri ya Makete
November 17, 2023, 6:53 pm
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Makete Mh. Christopher Fungo pamoja na viongozi wengine katika kikao cha baraza la madiwani. Picha na Ombeni Mgongolwa
Ili kuhakikisha maendeleo kwa wananchi yanawafikia hususani viongozi nao kuwajibika katika nafasi zao imeonesha utoro kwa baadhi ya watumishi imekuwa ikirudisha nyuma jitihada za serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Na Ombeni Mgongolwa.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Makete, limeridhia kufukuzwa kazi kwa watumishi watano amabo ni watendaji wa vijiji, kwa kutokuwepo kwenye maeneo yao ya kazi kinyume cha sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Akisoma taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Halmshauri ya wilaya ya Makete, Mhe. Christopher Fungo, amesema kuwa baraza limeridhia watumishi hao wafukuzwe kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria za kiutumishi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waheshimiwa madiwani katika kikao cha baraza la madiwani Makete
Mhe. Fungo amewataja watumishi hao ambao wamefukuzwa kazi baada ya kukiuka kanuni za kiutumishi Na. 57(1) ya kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2022, kuwa ni; Alex Ponela, Afisa Mtendaji wa kijiji (III), alikuwa mtoro kazini kuanzia tarehe 14/05/2022 hadi tarehe 14/06/2022, Mashaka Jackob Mwalemba, Afisa Mtendaji wa kijiji (III) ambaye alikuwa mtoro kazini kuanzia tarehe 19/07/2023 hadi tarehe 26/07/2023 siku ya kuandikiwa hati ya mashtaka na notisi, Musa Mwambapa Mwamgina, Afisa Mtendaji wa kijiji (III), ambaye alikuwa mtoro kazini kuanzia tarehe 16/09/2022 hadi tarehe 26/07/2023, siku ya kuandikiwa hati ya mashtaka na notisi, Kelvin Ngailo, Afisa Mtendaji wa Kijiji (II) yeye alichezea mfumo wa mapato (POS) ya halmashauri na kuiibia kiasi cha Tsh 4,261,500/= alizokuwa amekusanya kwenye mfumo wa kukusanyia mapato katika kijiji cha Ikuwo na Joseph Patrick Mwaluwega, tabibu msaidizi, ambaye alikuwa mtoro kazini kuanzia tarehe 08/09/2022 hadi 18/09/2023, siku ya kuandikiwa hati ya mashtaka na notisi.
Ikumbukwe kuwa leo Novemba 17,2023, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Makete limefanya kikao cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024, ikiwa ni kikao cha pili baada ya kufanya kikao cha kwanza hapo jana Novemba 16/2023.