Mkurugenzi Makete DC aendelea na ukaguzi wa miradi
September 23, 2023, 3:35 pm
Kufuatia changamoto ya kutokuwepo kwa Madarasa ya Awali shule ya Msingi Kinyika, Serikali imeamua kujenga miundombinu ya madarasa shuleni hapo
Na Furahisha Nundu
Mkurugenzi Mtendaji H/w Makete Willium Makufwe ameendelea na ukaguzi wa madarasa katika Shule mbalimbali Wilayani hapa
Makufwe akiwa ameongozana na Wataalamu wa Ujenzi, Mipango na Elimu Leo Septemba 23, 2023 amekagua ukamilishaji wa Vyumba viwili vya Madarasa ya Awali ya mfano katika Shule ya Msingi Kinyika.
Madarasa hayo yenye zaidi ya shilingi Milioni 69 yapo katika hatua za mwisho za ujenzi ili kuanza kutumika
Vilevile Mkurugenzi huyo na Wataalamu wamekagua ujenzi wa Vyumba vya Madarasa, Vyoo na Bweni katika Shule ya Sekondari Matamba ambapo Serikali imetoa fedha Kiasi cha shilingi Milioni 616 ili kujenga miundombinu katika Shule hiyo.
Miezi michache iliyopita Serikali ilitoa fedha zaidi ya Bilioni 2 Kwa ajili ya kujenga Vyumba vya Madarasa, Bweni na Vyoo katika Shule mbalimbali za Msingi na Sekondari Wilayani Makete ambapo Mkurugenzi Mtendaji H/w Makete na Wataalamu wake wamekuwa wakifuatilia ujenzi huo mara kwa mara kuhakikisha ujenzi wake unakuwa katika ubora unaotakiwa sambamba na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali
Shule zilizopata fedha hizo ni pamoja na Mwakavuta, Matamba, Kinyika Shule ya Msingi, Ighala Shule ya Msingi, Mlanda na Missiwa