Fedha zachangwa msibani kutatua changamoto ya barabara Makete
September 22, 2023, 8:57 am
Kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara katika kijiji cha Igolwa kilichopo wilaya ya Makete – Njombe wananchi wamelazimika kuchangisha fedha katika matukio mbalimbali ikiwemo misiba ili kujikwamua na changamoto hiyo.
Na Aldo Sanga.
Wananchi wa kijiji cha Igolwa wameomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto ya miundombinu ya barabara kutokana na adha wanazokumbana nazo ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha, kutumia muda mrefu kufuata huduma za afya, gharama za usafiri kuwa kubwa pamoja na huduma nyinginezo huku wakieleza kuwa kutoka kijiji cha Igolwa hadi mji wa Ikonda ni chini ya kilomita 40 ambapo hutumia zaidi ya Tsh:30,000/= hadi 40,000/= kulipia nauli kwa pikipiki.
Wakizungumza katika nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliojitokeza kufanya kazi ya kufukia mashimo ya barabara katika baadhi ya sehemu korofi, wamesema moja kati ya changamoto kubwa kijijini hapo ni ubovu wa miundombinu ya barabara ambapo hulazimika kuchangishana fedha na kutumia nguvu kazi kutengeneza barabara kwa mikono kufukia mashimo makubwa ili waweze kupita kufuata huduma mbalimbali katika vijiji vya jirani.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Bwana Edwin Sanga ameeleza jinsi baadhi ya wadau walivyoamua kuaanza kuchukua hatua za kusaidia juhudi za wananchi kwa kutoa magari yao na nguvu kazi,na kuongeza kuwa kwa sasa wamelazimika kuchangisha fedha wakati wa misiba inapotokea ambapo hadi sasa wamechangisha zaidi ya shilingi milioni mbili kwa ajili ya kutatua changamoto ya barabara.
Kijiji cha Igolwa ni miongoni mwa vijiji vilivyopo halmashauri ya wilaya ya Makete ambavyo vinategemea kupata mahitaji mbalimbali katika mji wa Tandala ambapo ni takribani kilomita 40, kwa sasa hutumia takribani saa 5-10 kwa msimu wa masika na msimu wa kiangazi saa 2-4 kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara wakati ni mwendo wa dakika 45 hadi saa moja ikiwa barabara zitaimarika.