Watanzania Tuenzi Mila na Desturi zetu-Mhe. Mkuchika
August 27, 2023, 7:58 pm
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum Mhe. Kapt Mstaafu George Mkuchika ameiasa jamii kuenzi mila na desturi za Tanzania ambazo ndio utambulisho wa Taifa hilo ndani na nje ya nchi, na kuacha kuiga utamaduni usiofaa wa Mataifa mengine.
Mhe. Mkuchika amesema hayo Agosti 27, 2023 Mkoani Njombe, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kufunga Tamasha la pili la Utamaduni lililokua na Kauli Mbiu “Utamaduni ni Msingi wa Maadili Tuulinde na Kuendeleza”
“Nawapongeza kwa kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambayo yanaenzi maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1962 alipozindua Wizara ya Vijana na Utamaduni ambapo alisema Taifa lisilokua na Utamaduni wake ni Taifa Mfu na ni sawa na mwili bila nguo” Mhe. Kapt Mstaafu George Mkuchika
Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema, lengo la Tamasha hilo ni kutoa fursa kwa Watanzania kuufahamu Utamaduni wa Tanzania kuusherehekea, kuutunza, na kuuendeleza utamaduni wao pamoja na kubadilishana utamaduni wa mkoa mmoja na mwingine.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema katika Tamasha hilo, shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwemo shindano la kuibua vipaji la Njombe Vibe, mbio za polepole (Jogging), mashindano ya vyakula na ngoma za asili, maonesho ya shughuli za utamaduni na sanaa, mdahalo wa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili pamoja maonesho ya filamu ya The Royal Tour katika kuunga mkono jitihada za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuitangaza Tanzania.
Katika Tamasha hilo Mkoa wa Mwanza umeibuka Mshindi wa kwanza wa Ngoma za asili ukifuatiwa na Dodoma na namba tatu ni Mkoa wa Njombe, ambapo pia katika mashindano ya vyakula vya asili Mkoa wa Kilimanjaro umeibuka Mshindi ukifuatiwa na Iringa.
Katika hatua nyingine Tamasha la tatu la Utamaduni Kitaifa mwaka 2024, litafanyika katika Mkoa wa Morogoro mwezi Agosti ambapo Mkoa huo umesisitizwa kujiandaa vyema.