Wanufaika TASAF Wakabiliana na Umasikini Makete
August 26, 2023, 12:50 pm
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ndulamo Remi Mahenge ameiomba Serikali kuendelea kuwasaidia walengwa wa Mradi wa kusaidia Kaya Masikini ili kuwanusuru na ugumu wa Maisha.
Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa Fedha kwa wanufaika wa Mradi huo Kitongoji cha Ndulamo Mji mdogo wa Iwawa, Mahenge amesema tangu kuanza kwa mradi huo kwenye Kitongoji hicho Maisha ya walengwa yamebadilika kwa kiasi kikubwa na wengi wao wameonesha dalili za kukabiliana na Umasikini kwa kujishughulisha na Kilimo, Ujasiriamali na ufugaji.
“Nishukuru Serikali kwa kuwasaidia wananchi wangu, kwa sasa hali ya Maisha kwa kila mmoja mmoja anayenufaika na TASAF inabadilika na wanaonyesha matumaini makubwa ya kupambana na Umasikini, niombe Serikali kuendelea kuwasaidia wananchi hawa ili waondokane kabisa na Umasikini”.
Bi. Selina Kawimbe na Asifiwe Mahenge ni miongoni mwa wafufaika wa mradi wa TASAF katika Kitongoji hicho wamesema fedha wanazopata zinawasaidia katika mambo mbalimbali ikiwemo ufugaji, ujasiriamali na kukidhi baadhi ya mahitaji ya wanafunzi pamoja na mahitaji ya nyumbani.