Elimu ya msaada wa kisheria yawafikia elfu 69 Makete
July 26, 2023, 9:20 pm
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la kutoa msaada wa kisheria wilayani Makete Mch. Denis Sinene amesema jumla ya wananchi elfu 69 wamefikiwa na elimu ya msaada wa kisheria wilayani Makete.
Mch. Sinene amesema hayo wakati wa kusoma taarifa ya utekelezaji wa mipango mikakati ya shirika hilo kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Januari-Juni 2023 akiwa na wasaidizi wa kisheria kutoka kata zote 23 za wilaya ya Makete, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Makete Ndg. Humphrey Mushi, Makamu Mwenyekiti wa Bodi Orgeni Sanga na Wadau mbalimbali wa Shirika hilo
Sinene amesema wananchi wameendelea kupata elimu namna ya upatikanaji wa haki, masuala ya ukatili wa kijinsia, changamoto za mgogoro ya ardhi kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara inayofanyika kwenye vijiji mbalimbali.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa kwa kipindi cha miezi 6 mwaka 2023 shirika hilo limepokea mashauri 218 ambayo yanahusu ndoa, migogoro ya ardhi, malezi ya watoto, unyanyasaji wa kijinsia na mambo mengine.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya MAPAO Orgeni Sanga, amesema shirika limekuwa likitoa msaada mkubwa kwa jamii ya wana Makete na nje ya Makete kwa kutoa elimu na msaada wa kisheria na kupelekea kupunguza changamoto mbalimbali pamoja na kupunguza gharama za kesi mbalimbali.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Makete Humphrey Mushi amesema uwepo wa shirika hilo wilayani Makete imekuwa mkombozi mkubwa kwa jamii katika utatuzi wa migogoro mbalimbali ambayo inajitokeza kwenye jamii na kusaidia kuitatua bila gharama yoyote…hivyo wasaidizi hao kisheria wanastahili kupongezwa.
Henry Nyigu Afisa Maendeleo na Msajili Msaidizi amelipongeza shirika hilo kwa kazi kubwa inayofanyika katika kutoa elimu kwa jamii ya Makete kwani imekuwa ikitoa msaada mkubwa kwa jamii kuhusu msaada wa kisheria.