Wizara ya Afya, TAMISEMI zapongeza huduma ya afya Makete
July 25, 2023, 8:19 am
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi (Afya) Dkt. Charles Mahera wameipongeza halmashauri ya wilaya ya Makete kwa kusimamia vizuri ujenzi wa hospitali ya wilaya na ukarabati wa majengo unaoendelea.
Makatibu wakuu hao wametoa pongezi hizo walipotembelea hospitalini hapo na kukagua ujenzi huo ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Viongozi hao wamesema ujenzi huo unaendelea vizuri na thamani ya fedha inaonekana katika majengo yanayoendelea kujengwa pamoja na ukarabati wanaoufanya kwenye baadhi ya majengo.
“Tumejionea samani zinazotumika kwenye ujenzi huu pamoja na vifaa vingine inaonesha jinsi mnavyosimamia fedha hizi zilizotolewa na Serikali kwa umakini…nikupongeze Mkurugenzi, Mganga Mkuu na watalaamu wote kwa usimamizi huu thabiti” Dkt. Magembe
“Serikali imenunua vifaa hivi vikubwa na muhimu kwa huduma ya wagonjwa, tunachotaka watalaamu wetu wawe na ujuzi wa kivitumia ili kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa na lengo la Serikali ni vifaa hivi vipatikane mpaka kwenye Zahanati ili wananchi wasipate changamoto ya huduma umbali mrefu” Dkt. Mahera
Dkt. Grace Magembe na Dkt. Charles Mahera pia wamekagua Duka la Dawa na namna dawa zinavyohifadhiwa na kutolewa pamoja na mifumo ya utoaji wa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Makete ambapo wamesema uhifadhi wa taarifa za wagonjwa uko vizuri na wanaitumia vizuri mifumo ya TEHAMA.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Makete Willium Makufwe amesema Serikali imetoa fedha zaidi ya Milioni 900 kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya Hospitali hiyo ambayo imekuwa chakavu kwa muda mrefu.
Pia Makufwe ameongeza kuwa Serikali imetoa fedha Milioni 300 kujenga jengo la dharula ambalo limekamilika na linatoa huduma tayari katika Hospitali hiyo huku akiishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wake.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Ligobert Kalisa amesema fedha zinazotolewa na Serikali wanahakikisha zinasimamiwa ipasavyo ili kutimiza adhma ya Serikali kwa kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma kwa wagonjwa.