CPB kununua ngano yote iliyozalishwa Makete
July 25, 2023, 8:16 am
Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko CPB imewathibitishia wakulima wa zao la ngano kununua ngano yote wilaya ya Makete mkoani Njombe iliyolimwa na wakulima ambayo itakuwa na ubora.
Akizungumza na wakulima wa kata za Kigala na Ikuwo Joel Mwanga kutoka Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko amesema serikali kupitia taasisi hiyo ya CPB imejipanga kununua zao hilo kutoka kwa wakulima kote wilayani Makete kwa bei watakayokubaliana.
Kwa upande wake Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Aniseti Ndunguru amesema ununuzi wa zao hilo utafanyika kwenye vituo vitakavyopagwa kwenye vijiji ambavyo kila mkulima anayehitaji kuuza ngano atauza hapohapo kijijini kwa kutumia mizani.
Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Makete Bi. Jackline Mroso amewataka vijana waliokopeshwa fedha za 10% kupitia halmashauri na kulima ngano kata ya Kigala kurudisha mkopo wao kiasi cha shilingi milioni 100 kwa lengo la kuwakopesha na wengine.
Baadhi ya wakulima wa zao hilo Stomeki Ng’wavi mkazi wa kijiji cha Kigala na Monica Ngajilo mkazi wa Kijiji cha Ikuwo wameiomba serikali kuweka vituo vya kununulia ngano karibu na maeneo yao ili kupunguza gharama za usafirishaji wa zao hilo.