Kilimo cha ngano kuwa mkombozi kwa wakulima Makete
June 21, 2023, 7:44 am
Shamba la mfano la Ngano Kijiji cha Kigala Wilaya ya Makete
Halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipago ya Matumizi ya Ardhi imezindua mkakati wa kupanga, kupima ardhi na kutoa hati za hatimiliki za kimila kwa wakulima wa ngano.
Mpango huo umezinduliwa na mkuu wa mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka wilayani Makete ambapo amesema jitihada za serikali ni kuhakikisha mkulima wa ngano anapata manufaa kupitia zao hilo.
Mhe. Mtaka amesema serikali kupitia Wizara ya Kilimo iligawa mbegu bora kwa wakulima wilaya ya Makete tani 80 mnamo mwezi Februari 2023, ambazo wakulima wamepanda na wanatarajia kupata matokeo siku chache zijazo.
Vilevile ameongeza kwa kuwapongeza wadau wa kilimo nchini wakiwemo TARI Uyole na TARI Mlingano, ASA, SUA, CPB, CRDB, NMB, Wakala wa mbegu nchini kwa kuwasaidia wakulima wa Makete ambao wanatarajia kuona matunda ya Kilimo miezi michache ijayo.
Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya Makete William Makufwe akiwa kwenye hafla hiyo amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 halmashauri imetenga fedha zaidi ya milioni 400 kwa ajili ya kuwakopesha wakulima wilayani Makete.
Pia amesema halmashauri kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo imeanzisha na kusimamia mashamba ya majaribio ya ngano katika kata za Matamba na Kigala.
Huku akibainisha kuwa halmashauri kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi itafanya mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji 44 katika kata za Kipagalo, Luwumbu, Bulongwa, Ikuwo, Iniho, Kigala, Ipelele, Matamba na Itundu.
Makufwe amesema halamshauri imepanga kuongeza idadi ya wakulima wa zao la ngano kutoka 19,796 waliopo sasa hadi kufikia 40,250 mwaka 2026, huku mapato yatokanayo na ushuru wa ngano yakiongezeka kutoka milioni 1 hadi milioni 690 ifikapo 2026.
Diwani wa kata ya Tandala Mhe. Daniel Hatanaka kwa niaba ya madiwani ameipongeza serikali kwa kutoa bure mbegu za ngano kwa wakulima huku akiziomba taasisi mbalimbali za kifedha kuwakopesha wakulima ili waweze kupata pembejeo za kisasa na kuongeza uzalishaji wa mazao kibiashara.
Kwa upande wake afisa tarafa ya Lupalilo Augustino Ngailo amewashukuru mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, mkurugenzi mtendaji H/W ya Makete na wataalam kwa kuwa na mawazo mapana ya kuwasaidia wananchi kupitia zao la ngano.