Milioni 133 kujenga nyumba za walimu, madarasa na vyoo shule ya msingi Missiwa
June 13, 2023, 8:16 am
Kupitia mradi wa BOOST serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 183 ili kujenga madarasa 3, nyumba 1 ya 2 in 1 ya walimu na vyoo matundu 4 shule ya msingi Missiwa kata ya Ipelele, wilaya ya Makete mkoani Njombe.
Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Makete akiwa ameongozana na wataalam mbalimbali leo Juni 12, 2023 wamekagua ujenzi wa madarasa, nyumba na vyoo na kuwataka mafundi kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Wakati huohuo amewataka wajumbe wa kamati ya manunuzi kuongeza kasi ya manunuzi huku wakizingatia taratibu zote za manunuzi kwa umakini ili kutoingizia hasara serikali.
Diwani kata ya Ipelele Mhe. Napeti Sigala ameahidi kushirikiana kikamilifu na wataalam kuhakikisha fedha hizo zinatumika vizuri ndani ya muda uliopangwa.
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi shule ya msingi Missiwa Jainosi Chungu amesema wanaishukuru serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha hizo kwani shule hiyo ilikuwa na miundombinu chakavu sana na sasa wanakwenda kubadilisha mazingira hayo na kuwa ya kisasa zaidi.