Mfumko bei ya viazi: Wadau walalamikia gharama za chips Makete
June 9, 2023, 7:41 am
Imeelezwa kuwa kitendo cha viazi kupanda bei kutoka shilingi elfu 12 hadi shilingi elfu 15 kwa debe moja, baadhi ya wateja na wafanyabiashara wa chipsi hapa Makete mjini wamelalamikia kuuziwa chips kidogo na kutopata faida yoyote kwenye biashara hiyo.
Estuda Mbilinyi pamoja na Nestory Sanga ni wafanyabiashara wa chips hapa Makete mjini wameiambia Kitulo FM kwamba kama bei ya viazi imepanda basi wanaiomba mamlaka husika iweze kupandisha bei ya chipsi kwa sahani kutoka bei ya sasa ya shilingi elfu moja hadi elfu moja na mia tano au 2000.
Baadhi ya wakulima akiwemo Faraja Sanga kutoka kijiji cha Ivilikinge amesema bei ya viazi imekuwa ikibadilika mara kwa mara ambapo wao kama wakulima wanashindwa kudhibiti bei hiyo.
Wilaya ya Makete ni miongoni mwa wilaya zinazozalisha viazi kwa wingi nchini hasa katika kata za Kitulo, Isaplano, Ipelele na kata zingine lakini wakulima pamoja na wafanyabiashara wamekuwa hawana uwezo wa kudhibiti bei ya zao hilo kutokana na mfumo wa uendeshaji wa biashara hiyo.