Wito: Maafisa ugani tembeleeni wakulima shambani
June 8, 2023, 2:03 pm
Wakulima wilayani Makete mkoani Njombe wametakiwa kuendelea kuwatumia maafisa ugani waliopo katika maeneo yao katika shughuli zao za kilimo ambapo nao maafisa ugani wakitakiwa kuendelea kuwatembelea wakulima na kutoa elimu juu ya masuala ya kilimo bora ili kiweze kuwa na tija kwa wakulima.
Hayo yamesemwa na kaimu mkuu wa idara ya kilimo mifugo na uvuvi kutoka wilayani Makete Bwana Ahamadi Kichombaki wakati akielezea maendeleo ya kilimo cha ngano kwa wakulima iliyosambazwa kwenye baadhi ya kata hapa wilayani Makete, ngano ambayo ilitolewa na serikali tani 80 kwa ajili ya kuwagawia wakulima.
Aidha amesema kuwa wao kama idara ya kilimo pamoja na halmashauri bado wana mikakati mikubwa ya kuendelea kuwasimamia wakulima katika hatua zote za uzalishaji wa ngano hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya uvunaji na utunzaji wa mbegu hiyo ili kufikia malengo ya wilaya ya Makete kulima ngano kwa wingi .
Kwa upande mwingine amewataka wakulima waliopata ngano hiyo kuendelea kufuata elimu na maelekezo wanayopatiwa na watalaam wa kilimo kwenye maeneo yao ili wapate tija kwenye kilimo hicho na amewataka kuacha kulima kilimo cha mazoea kwani mbegu hiyo inahitaji kufuata kila kanuni zote za kilimo na imeshafanyiwa majaribio kwenye maeneo mbalimbali.
Ikumbukwe kuwa halmashauri ya wilaya ya Mkete ilipokea tani 80 za mbegu za ngano mwezi wa Februari mwaka huu kutoka serikalini na ilisambazwa kwenye baadhi ya kata zake kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa zao la ngano ili kuweza kufikia malengo ya wilaya ya Makete kuwa miongoni mwa wazalishaji wa zao hilo kwa wingi hapa nchini.