Zimamoto: Wananchi kuwa makini uchomaji moto kipindi cha kiangazi
June 8, 2023, 10:29 am
Wito umetolewa kwa wananchi wilayani Makete mkoani Njombe kuwa makini na uchomaji moto maeneo mbalimbali hasa katika kipindi cha kiangazi
Wito huo umetolewa na Stesheni Sajenti EVALISTO MG’ONG’O ambaye ni Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji wilaya Makete ambapo amesema katika kipindi hiki cha kiangazi baadhi ya wananchi huandaa mashamba yao kwa kuchoma moto na baadhi yao moto umekuwa ukitoroka na kuteketeza mali za watu ikiwemo misitu.
Ametaja baadhi ya sababu zinazopelekea moto kutoroka na kuunguza maeneo ya watu ikiwemo hujuma kwamba mtu anaamua kwa maksudi kuchoma msitu wa mtu pamoja na baadhi ya watu wanaovuta sigara.
Katika kipindi cha kiangazi wilaya ya Makete hukumbwa na baridi kali hasa nyakati za jioni na kupelekea baadhi ya wananchi kulala na jiko lenye moto hasa jiko la mkaa ndani ya nyumba zao, Kamanda Mng’ong’o amewataka wananchi kutofanya hivyo kwani ni hatari kwa maisha yao.
Pamoja na mambo mengine amewataka wananchi kutoa taarifa pindi majanga ya moto yanapotokea kwa kupiga simu bure kwenda namba 114