Tani 80 za Ngano zapokelewa Makete
Kitulo FM

Tani 80 za mbegu ya ngano zapokelewa Makete

March 3, 2023, 2:47 pm

Halmashauri ya Wilaya ya Makete imepokea Tani 80 za Mbegu ya Ngano kutoka Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo ASA kwa ajili ya kugawa kwa wakulima wa zao hilo Wilayani hapa.

Akizungumza mapema leo kwenye zoezi la makabidhiano ya Mbegu hizo za Ngano Afisa Kilimo kutoka ASA Bi. Aneth Molela amesema Serikali imetoa mbegu hizo kwa lengo la kugawa kwa wakulima ili wazalishe kwa tija na kibiashara zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda amesema Wilaya ya Makete itakuwa Wilaya Mama kwa kilimo cha ngano nchini na Hekta zaidi ya 6,000 zimepimwa kwa ajili ya Kilimo cha ngano

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Makete Clement Ngajilo amesema Serikali inafanya yote hayo kuhakikisha inaboresha maisha ya wananchi hususani wakulima wadogo na Kilimo cha ngano itakuwa mkombozi kwa wakulima kwani tayari miundombinu ya Barabara imeanza kufunguka pande zote

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Mhe. Hawa Kader amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Kilimo kwa kuleta mbegu bora kwa wakulima huku akiwasihi wakulima kufanya kilimo cha kisasa

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Makete William Makufwe amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri imetenga fedha zaidi ya Milioni 500 kwa ajili ya kilimo cha ngano na kuwakopesha vijana na wanawake kwa ajili ya kuboresha kilimo cha ngano Wilayani hapa.

Afisa Kilimo Wilaya ya Makete Aniseth Ndunguru amesema Halmashauri imejipanga vizuri kuhakikisha wakulima wananufaika na Kilimo hicho na tayari wameshachukua sampuli za Ardhi kupelekwa maabara ili wakulima waweze kufanya kilimo cha Faida

Baadhi ya wakulima waliofika kupokea Mbegu hizo wameishukuru Serikali ya Jmahuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajali wakulima na kutambua umuhimu wa Kilimo cha Ngano katika Wilaya ya Makete

Zoezi la kupokea ngano likifanyika nje ya Makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Makete