Nchi ya Haiti yaja Njombe kujifunza Mbinu za utoaji wa Chanjo ya Uvico 19
January 27, 2023, 10:56 am
Serikali ya Hait toka Amerika ya kusini imetuma wajumbe wake kuja kujifunza katika wilaya ya Njombe namna ilivyofanikiwa katika utekelezaji wa utoaji wa Chanjo ya UVICO 19 kupitia kampeni maalum ya kijiji kwa kijiji chini ya mkuu wa Wilaya ya Njombe.
Akizungumza baada ya majadiliano ya namna kampeni hiyo ilivyofanikiwa Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amesema mbinu aliyoitumia katika kampeni hiyo ya kuhamasisha jamii kupata chanjo ya UVICO 19 kwa kufanya mikutano kijiji kwa kijiji pamoja na wataalamu wa Afya ndiyo iliyosababisha kupata mafanikio makubwa.
Kwa upande wake mkurugenzi mwakilishi wa serikali ya Hait katika mradi wa Fhi360 Dokta Magda Cheron anasema walivutiwa kuja kujifunza wilayani Njombe mbinu zilizotumika kuhamasisha jamii kuchanja chanjo ya uviko 19 kutokana na takwimu kuonesha mafanikio makubwa na kulazimika kusafiri siku mbili angani kwa ndege.
Mganga mkuu wa mkoa wa Njombe Dokta Juma Mfanga amekiri kuwa Njombe ilifanya kazi kubwa ya kufanikiwa utoaji wa Chanjo ya UVIKO 19 kwani walifikia asilimia 100 katika kipindi cha miezi 15 ikiwa nchi ya Hait katika kipindi cha miaka miwili walifikia asilimia 5 pekee katika utekelezaji wake na kusababisha wageni hao kufika wilayani Njombe.
Baadhi ya wakazi wa Njombe akiwemo Dokta Baraka Alinan na Erasto Komba wamesema awali kulikuwa na changamoto ya hofu kwa watanzania wengi juu ya chanjo ya Uviko 19 lakini baada ya elimu jamii ilihamasika na kuchanja.
Ugonjwa wa Corona uliibuka mwaka 2019 huko nchini China na kusambaa kwa kasi duniani kote jambo lililosabisha mamia ya watu kufariki dunia kwa kukosa dawa.