Kitulo FM

Miti 5,000 ya Asili yapandwa Kijiji cha Ihela

January 20, 2023, 7:23 pm

Wananchi wilayani Makete mkoani Njombe wametakiwa kutunza mazingira ikiwemo vyanzo vya maji ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo kuongezeka kwa joto duniani,ukame pamoja na kubadilika kwa msimu wa mvua.

Wito huo umetolewa January 20,2023 na Agustino Ngailo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya uzinduzi wa upandaji miti kiwilaya akimwakilisha mkuu wa wilaya ya Makete Mh.Juma Sweda yaliyofanyika katika chanzo cha maji kilichopo eneo la Ichange karibu na Zahanati ya kijiji cha Ihela ambapo jumla ya miti 5,000 ya asili na rafiki kwa vyanzo vya maji imepandwa katika vyanzo vya maji vya Ichange na Ilungu A

Naye kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete Upendo Mgaya ambaye pia ni afisa mazingira wilaya ya Makete amewapongeza wananchi wa kijiji cha Ihela kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo huku pia akitoa wito kwa wananchi kuitunza miti hiyo ikiwa ni pamoja na kuheshimu sheria zilizopo ili vyanzo hivyo viwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho

Nacho Chama cha mapinduzi (CCM) katika salamu zake kimeiomba serikali kuhakikisha inashughulikia suala la kuondoa miti aina Paina karibu cha chanzo hicho cha maji pamoja na kuhakikisha wale wote wanaoendelea kufanya shughuli za kilimo karibu na chanzo cha maji cha Ichange wanasitisha mara moja

Huruma sanga ni Mwenyekiti wa kijiji cha Ihela amelishukuru shirika la SUMASESU na halmashauri ya wilaya ya Makete kwa jitihada zake huku afisa mtendaji wa kata ya Tandala Maximlian Msigwa akiahidi kuyasmimia maelekezo yote yaliyotolewa na watalaamu.

Kwa upande wake mratibu wa zoezi la tathmini ya majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi kutoka Shirika la SUMASESU Joyce Kayila baada ya kushiriki zoezi la kupanda miti hiyo amesema kuwa tangu kuanza kwa zoezi hilo lililoanza mwaka 2022 katika kijiji cha Ihela wamekuwa na ushirikiano mzuri na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Makete huku akiishukuru kwa kutoa miche ya miti ya asili 5000 katika kijiji hicho.