Kitulo FM

AFUNGWA MIAKA 30 WILAYANI LUDEWA KWA KOSA LA UBAKAJI

January 19, 2023, 8:03 am

Mahakama Wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe Januari 17, 2023 imemhukumu kifungo cha Miaka 30 jela Daudi David Mligo, mwenye umri wa miaka 26, mkazi wa Ludewa Mjini baada ya kukutwa na kosa la ubakaji.

Mnamo Julai 16, 2022 majira ya saa tisa na dakika 15 alasiri katika kituo cha Polisi cha Wilaya, iliripotiwa taarifa kwamba mtuhumiwa huyo alimbaka mlalamikaji (jina limehifadhiwa)

Baada ya upelelezi kukamilika mtuhumiwa alifikishwa katika mahakama ya wilaya Ludewa, mnamo 26 Julai 2022 ambapo alisomewa mashitaka mawili ya kubaka na kujeruhi, mbele ya Mwendesha Mashtaka wa serikali g.3616 d/cpl Angelo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya Ludewa, Isaac Ayeng’o na mtuhumiwa alikanusha kutenda kosa ndipo upande wa Jamhuri ulileta mashahidi.

Mshitakiwa alikutwa na kesi ya kujibu na kutakiwa ajitetee na baada ya mshitakiwa kujitetea Mahakama ya wilaya Ludewa, mbele ya Hakimu Isaac Ayeng’o ilikaa na kupitia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili yaani upande wa Jamhuri na upande wa utetezi Mahakama ilijiridhisha kuwa upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kosa pasipo kuacha shaka yoyote na hivyo ilimkuta mshitakiwa na hatia kwa makosa yote mawili.