Kitulo FM

Waiomba Serikali kunusuru wanafunzi kupigwa na Radi

January 17, 2023, 9:31 am

 

Wananchi wa Kijiji cha Ihela Kata ya Tandala Wilayani Makete wameiomba Serikali kuangalia chanzo cha radi eneo la shule ili kuepusha hatari ya watoto kupigwa radi

Wakizungumza na Kitulo Fm kwa nyakati tofauti wananchi hao wameeleza kuwa kumekuwa na moto wa radi unaojitokeza mara kwa mara kwenye uwanja wa mpira ulio karibu na shule ya Msingi Ihela
Huruma Sanga na Matesi Mbilinyi wakazi wa Kijiji hicho wamesema wananchi wamekuwa wakishuhudia moto ukiwaka kwenye miti ya magoli iliyosimikwa katika uwanja wa mpira mara kwa mara kunapokuwa na mvua inayoambatana na radi.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Ihela Josephati Nuje amesema ni kweli matukio ya radi yamekuwa yakishuhudiwa mara kwa mara uwanjani na kuongeza wasiwasi juu kutokea kwa hatari endapo kutakuwa na watoto wakicheza eneo hilo na amekuwa akitoa taarifa uongozi wa Kijiji na Wilaya juu ya uwepo wa matukio hayo kila yanapotokea.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ihela Huruma Sanga amesema kwa mwaka huu 2023 januari kumetokea matukio mawili kwa siku tofauti eneo hilohilo na kila mwaka lazima itokee hivyo ameiomba Serikali kufanya utafiti wa eneo hilo ili kujua chanzo ni nini kwa lengo la kunusuru uhai wa wanafunzi wanaokuwa eneo hilo muda mwingi.