Kitulo FM

Msako kuanza kwa Wazazi/Walezi ambao hawajapeleka Wanafunzi Shule

January 9, 2023, 5:27 pm

 

Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda amesema msako mkali utafanyika kwa wazazi/walezi ambao hawatapeleka wanafunzi shuleni

Wanafunzi Kidato cha kwanza na darasa la kwanza wameanza kuripoti shuleni katika shule mbalimbali Wilayani Makete huku Mkuu wa Wilaya akiagiza kukamatwa kwa Mzazi yeyote ambaye hataki kupeleka mwanafunzi shuleni.

Leo tarehe 9 Januari, 2023 Akiwa katika ukaguzi wa mapokezi ya wanafunzi hao upande wa Elimu Sekondari Mhe. Sweda ameeleza kutoridhishwa na kasi ya wazazi ndogo ya wazazi/walezi kupeleka watoto shuleni

Mhe. Sweda amefanya ukaguzi huo shule ya Sekondari Iwawa, Ilumaki, Lupalilo na Mang’oto ameagiza kuanzia Jumatano wiki kuanza msako mkalai kwa Mzazi/Mlezi ambaye atakuwa hajampeleka mtoto shuleni ili akamatwe na kufikishwa Mahakamani kujibu mashtaka

Kwa upande wa shule ya Sekondari Iwawa, Kaimu Mkuu wa shule hiyo Mwl. Jitahidi Sanga amesema mapokezi kwa wanafunzi yamekuwa mazuri na anatarajia kufikia Jumatano tarehe 12 Januari, 2023 wanafunzi wote watakuwa wameripoti shuleni.

Baadhi ya Wazazi waliozungumza na Kitulo FM Suzana Sanga kutoka Ilumaki Sekondari na Mendrad Mwinuka kutoka Mang’oto Sekondari wameeleza kufurahia kupeleka watoto wao Sekondari huku wakiwasihi wazazi wenzao ambao bado hawajapeleka wanafunzi shuleni kuhakikisha wanafuata utaratibu na miongozo ya Elimu ili kukwepa mkondo wa sheria.

Siku chache zilizopita Mkuu huyo wa Wilaya aliagiza kukamatwa kwa mzazi yeyote ambaye atabainika kumtorosha mwanafunzi ili kufikishwa kwenye vyombo vya sheria au aingie mzazi Darasani kusoma kwa niaba ya mwanafunzi.