Kitulo FM

Wanafunzi 17 wanunuliwa vifaa kujiunga na Kidato cha Kwanza Iwawa Sekondari

January 6, 2023, 5:49 pm

 

Mwanafunzi aliyehitimu Darasa la saba 2022 akipokea Cheti kutoka kwa Mkurugenzi wa GNM Cargo Ndg. Jofrey Mbilinyi

Mbunge Jimbo la Makete Mhe. Festo Sanga kwa kushirikiana na Jofrey Mbilinyi Mkurugenzi wa GNM CARGO wamekabidhi vifaa kwa wanafunzi 17 waliomaliza shule ya Msingi Maleutsi Kata ya Iwawa Wilaya ya Makete na kufanikiwa kujiunga kidato cha kwanza.

Vifaa hivyo ni pamoja na sare za Shule, nguo za michezo, Madaftari ikiwa ni pamoja na kuwalipia michango yote ya shule ili kuwarahisishia wazazi kutopata changamoto ya kushindwa kupeleka watoto kidato cha kwanza Januari 9, 2023.

Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maleutsi Turuka Mahenge amesema hakuna haja ya mwanafunzi kushindwa kwenda kuanza masomo ifikapo jumatatu tarehe 9 januari kwani kila kitu ameshaandaliwa.

Prisca Mahenge na Amani Mbilinyi wazazi wa wanafunzi hao wamemshukuru Mhe. Mbunge na GNM CARGO kwa kuwasaidia kununua vifaa vya shule na kuchangia michango yote ya shule kwani wamewapunguzia mzigo kwa kiasi kikubwa.