Kitulo FM

Daraja lasombwa na Maji Mwakauta-Makete

January 4, 2023, 9:31 am

 

Picha ya Daraja

Daraja la Mbao lililokuwa likitumiwa na watembea kwa miguu wanaovuka kutoka Kijiji cha Mwakauta kwenda kupata huduma za Afya Hospitali ya Bulongwa limesombwa na Maji baada ya mvua kubwa kunyesha siku kadhaa zilizopita.

Ni siku 5 zimepita wananchi wa Kijiji hicho cha Mwakauta na Vijiji vingine kama Lumage wanashindwa kuvuka Mto Luvanyina lilipojengwa daraja hilo na kulazimika kuzunguka umbali mrefu kwa kutembea kwa miguu au kukodi pikipiki ili kufika Hospitalini kupata huduma.

Jailo Mbogela na Nipokee Sanga wamesema kwa sasa wanalazimika kutumia gharama kubwa kukodi pikipiki kwa shilingi 12,000 au kupanda gari kwa zaidi ya 5,000 kutoka vijiji vya mbali na Mwakauta ili kufika Hospitalini na kuomba wananchi wajitokeze mapema ili waweze kushirikiana kujenga upya daraja hilo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwakauta Kata ya Iniho Ndugu Nelson Tweve amesema kumetokea changamoto hiyo kwa zaidi ya siku 5 sasa na wananchi wanalazimika kutumia gharama kubwa kusafiri.

Mwenyekiti huyo amesema wameanza mpango wa kuandaa miti mikubwa na kuisogeza eneo ambapo Daraja lilijengwa waweze kujenga upya.

Kwa upande wake Daktari John Mcheshi moja ya viongozi wa Hospitali inayomilikiwa na Taasisi ya KKKT-DKK Bulongwa amesema wananchi wanakutana na gharama kubwa ili kufika Hospitalini kwa kutumia usafiri wa pikipiki au gari baada ya daraja hilo kusombwa na maji.

Dk. Mcheshi amesema Hospitali ipo tayari kutoa mbao na misumari ili kuongeza nguvu kwa wananchi waweze kujenga daraja hilo muhimu kwa wananchi wa Mwakauta, Lumage na Bulongwa.