Kitulo FM

Wananchi wabeba Tofali kujenga Bwalo la Wanafunzi Sekondari

January 3, 2023, 8:01 pm

 

Wananchi wakiweka tofali walizobeba kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Bwalo

Wananchi wa Kata ya Iniho Wilaya ya Makete wameshiriki katika kazi ya kusogeza tofali kwa ajili ya ukamilishaji ujenzi Bwalo la Shule ya Sekondari Mwakavuta baada ya changamoto ya barabara na magari ya mizigo kushindwa kufikisha vifaa eneo la ujenzi.

Zoezi hilo limefanyika leo Januari 3, 2023 na Wananchi hao kutoka katika vijiji vitano vya Kata hiyo ambavyo ni Lumage, Iniho, Mwakauta, Kidope na Unyangogo.

Veroniva Chaula Mkazi wa Kijiji cha Unyangogo amesema wamekuwa na kazi hiyo ya maendeleo kwa ushirikiano mkubwa wa wananchi wa vijiji vyote kwa lengo la kufanikisha ujenzi huo ili kuondokana na adha ya wanafunzi kula chakula kwenye jua au mvua, na bwalo hilo litatumika kwenye shughuli mbalimbali ikiwemo sherehe, makongamano na mikutano.

Rabson Luvanda Mwenyekiti wa Kijiji cha Iniho amesema kukamilika kwa bwalo hilo kutasaidia wanafunzi kufurahia mazingira ya kupata elimu na chakula wakati wote katika eneo salama.

Diwani wa Kata ya Iniho Mhe. Christopher Fungo akiwa na wananchi hao, amewapongeza kwa ushirikiano na mwamko walionao wananchi katika shughuli za Maendeleo na kuiomba Serikali kukarabati barabara ya Mwakauta kijijini mpaka kufika Mwakavuta Sekondari ili iweze kupitika wakati wote na kurahisisha shughuli za usafirishaji wa vifaa na wanafunzi pia.

Serikali imetoa fedha Milioni 100 kusaidia ujenzi wa bwalo ambapo wananchi walianza mwaka 2019 kwa kuchimba msingi, kuandaa mawe trip 5 kila kijiji na shule kupitia kuuza msitu wake ilikuwa ikifanya kazi ya kununua tofali na kusogeza mawe ya ujenzi.