Kitulo FM

Barabara ya Lami Km 36 kujengwa Makete

December 29, 2022, 7:45 am

Utiaji saini ujenzi wa Barabaraba ukifanyika Ukumbi wa Madihani Villa Makete Mjini

Barabara ya Makete-Mbeya kufunguka kwa lami Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara za lami katika mikoa ya nyanda za juu kusini ili kuunganisha vema ukanda huo na bandari ya Mtwara na hivyo kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji, kukuza uzalishaji wa mazao ya kilimo, misitu na kukuza utalii.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini ujenzi wa barabara ya Isyonje-Kikondo hadi Makete KM 96.2 sehemu ya Kitulo hadi Iniho KM 36.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami Waziri Prof. Mbarawa amesema Serikali ya awamu ya sita itahakikisha inaunganisha kwa njia fupi mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Njombe hadi Mbeya kupitia Makete ili kukuza fursa za kiuchumi zilizoko katika ushoroba huo.

 

Ameitaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kumsimamia kikamilifu Mkandarasi anayejenga barabara hiyo M/S China National Aero-Technology Egineering Corporation ili mradi huo ukamilike kwa wakati na viwango.

Mtendaji mkuu wa TANROADS Mhandisi Rogatus Mativila amesema ujenzi wa barabara hiyo utahusisha ujenzi wa mizani katika Kijiji cha Igalala ili kudhibiti magari yanayozidisha uzito hivyo kuwataka wananchi kuzingatia sheria na kulinda miundombinu yote ya barabara.

Kwa upande wake Mbunge wa Makete Festo Sanga ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo kwani kukamilika kwake kutaunganisha wilaya hiyo na Mkoa wa Mbeya kwa njia fupi, kukuza utalii wa hifadhi ya taifa Kitulo na kupandisha thamani ya mazao mbalimbali yanayozalishwa Mkoani Njombe.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Bw, Anthon Mtaka amewataka wakazi wa wilaya ya Makete kutumia maendeleo ya ujenzi wa miundombinu kuwekeza wilayani humo. Zaidi ya shilingi bilioni 69.7 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo wa Barabar ya Lami na Zege kwa muda wa Miezi 36.