Wananchi waondolewa hofu baada ya kuwepo kwa taarifa za kuweka sumu kwenye kisima cha maji
December 11, 2022, 8:27 am
Mhandisi Sanga akiwa Kijiji cha Ng’onde Kata ya Mlondwe
Mhandisi Sanga akiwa Kijiji cha Ng’onde Kata ya Mlondwe
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amewatoa hofu wananchi wa Mlondwe baada ya kuwepo taarifa za mtu kuweka sumu kwenye kisima cha maji Kijiji cha Mlondwe Wilaya ya Makete Mkoani Njombe.
Akizungumza tarehe 11 Disemba, 2022 na Viongozi wa Kijiji cha Mlondwe na Ng’onde Kata ya Mlondwe amesema baada ya taarifa hizo kusambaa wataalamu kutoka Iringa wamechukua maji hayo na kuyapima ambapo wamebaini hakuna sumu yoyote kwenye maji hayo kama ilivyoelezwa na watu wenye nia mbaya
Mhandisi Sanga amesema baada ya kutokea taarifa katika mitandao ya Kijamii kuhusu maji ya Kisima kuwekwa sumu Kijiji cha Mlondwe, Wizara ilichukua hatua za haraka kufuatilia uhakika wa taarifa hiyo na baada ya vipimo vya maabara imebainika maji hayo hayana sumu na ni salama kwa matumizi ya binadamu na wanyama wengine ikiwemo mifugo.
Diwani Kata ya Mlondwe Mhe. Alphonse Salimo amesema ugovi wa Mashamba baina ya watu wawili ammbao mmoja aliyeshindwa kesi kwenye baraz la kata la ardhi ndiye aliyesambaza taarifa hizo za uongo ndio sababu iliyopelekea kuanzisha uvumi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda ameagiza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa mtu aliyesambaza taarifa za kuwepo kwa sumu katika kisima cha maji huku akiwasihi wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa yao na Taifa sio kusambaza taarifa zinazoweza kuleta taharuki kwa wananchi
Wananchi wa Kijii cha Mlondwe wameipongeza Serikali kuchukua hatua za haraka kupima maji hayo jambo ambalo wameeleza kushtushwa na taarifa zilizosambazwa huku wakisema kwamba mhusika aliyesambaza taarifa hizo hana nia njema na wananchi wa Kijiji hicho ikiwa mhusika huyo haishi kijijini hapo na anafanya shughuli zake Jijini Dar Es salam.