Wazee Makete waishukuru Serikali kuelekea sherehe za Uhuru Disemba 9, 2022
December 5, 2022, 2:19 pm
Wazee maarufu Wilaya ya Makete wameishukuru Serikali kwa kuwajali katika huduma za kiafya na shughuli mbalimbali za kimaendeleo tangu nchi ipate uhuru wake mwaka 1961.
Wakizungumza na Kitulo FM Disemba 5, 2022 katika mdahalo ulioandaliwa na Kituo hiki ukiwahusisha wazee maarufu kuelekea Maadhimisho ya kufikisha miaka 61 ya Uhuru, wazee wao wamesema Serikali imeongeza kasi ya kuwajali wazee hususani katika huduma za Afya, miundombinu ya Elimu kwa watoto, uboreshaji wa huduma za maji kwa jamii na hata miundombinu ya barabara.
Mzee Samweli Makotso kutoka Mji mdogo wa Iwawa amesema, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya Afya na huduma za wazee wanapokwenda kupata huduma hizo katika Hospitali za Serikali na Hospitali binafsi kwani wanapata huduma haraka tofauti na miaka ishirini au thelathini iliyopita.
“Kwa kweli Serikali yetu tangu enzi za Mwalimu Nyerere imeonesha mabadiliko makubwa katika sekta ya Afya, sisi wazee tunapata huduma kwa urahisi tunapofika Hospitalini iwe hapa Hospitali ya Wilaya au Hospitali ya Mission Ikonda tunapewa kipaumbele… kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali yetu na pia tunashuhudia Serikali inajenga vituo vya Afya kila Tarafa katika Wilaya yetu”.
Mwenyekiti wa Wazee Wilaya ya Makete Frida Sanga amesema, kumekuwa na maboresho makubwa katika sekta ya Elimu tangu nchi ipate uhuru ambapo wameona ongezeko kubwa la shule za Sekondari kila kata, Maboresho ya madarasa katika shule za Msingi na hata katika vyuo mbalimbali nchini.
“Elimu yetu imezidi kukua kila ngazi kuanzia Elimu ya Msingi tunaona madarasa yanajengwa na kuboreshwa, lakini elimu ya Sekondari tunashuhudia sasa kila Kata imekuwa na Sekondari na wanafubnzi hawapati usumbufu kama tulivyosoma sisi miaka ya nyuma”