Kitulo FM

AHUKUMIWA MIAKA 8 JELA

October 23, 2021, 9:23 am

Mahakama ya Wilaya ya Makete Mkoani Njombe

Bw. Andrew Alfred Mbogela (29) mkazi wa Uyole jijini Mbeya amehukumiwa kwenda jela kifungo cha miaka 8 kwa kosa la wizi Ikulu ndogo Makete

Mshtakiwa huyo amekutwa na hatia katika mashtaka mawili ambapo katika shitaka la kwanza ameshtakiwa kwa kosa kuvunja nyumba usiku kwa nia ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 294(1)(2) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo 2019

Katika shitaka la pili mshtakiwa huyo ameshtakiwa kwa kosa la Wizi kinyume na kifungu cha 265 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo 2019

Katika shauri hilo la jinai namba 42 la mwaka 2021 imeelezwa mshtakiwa alitenda makosa yote mawili Juni 22, 2021 katika kijiji cha Iwawa wilayani Makete mkoani Njombe ambapo alivunja Ikulu Ndogo ya wilaya hiyo na kuiba Televisheni 1 (Flat Screen) yenye thamani ya sh. 600,000/-, Godoro 1 inchi 10 lenye thamani ya sh. 300,000/-,Jiko la Gesi na Mtungi wake la sh. 280,000 na mablanketi manne yenye thamani ya shilingi 480,000/-

Akitoa hukumu hiyo Oktoba 21, 2021 Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Makete Mh. Ivan Msaki amesema mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na kumtia hatiani mshtakiwa kwa makosa yote mawili

Kwa upande wa waendesha mashitaka wa serikali ambao ni Inspekta wa Polisi Benstad Mwoshe na Asifiwe Asajile wameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine hasa ukizingatia Ikulu ni jengo nyeti na lenye manufaa kwa umma na ni kwa ajili ya matumizi viongozi wakubwa wa serikali

Mshtakiwa huyo alipopewa nafasi ya kuomba mahakama impunguzie adhabu amesema anategemewa na mzazi wake ambaye alipata ajali na ana mke na watoto wanaomtegemea na wanasoma hivyo kuomba mahakama hiyo imhurumie

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mh. Msaki amemhukumu mshtakiwa huyo kwa kosa la kwanza la kuvunja nyumba Usiku kwa nia ya kuenda kosa kifungo cha miaka 5 jela na kwa shtaka la pili la wizi, akatumikie kifungo cha miaka mitatu jela na adhabu zote zitakwenda kwa nyakati tofauti.