Highlands FM
Highlands FM
11 November 2026, 1:50 pm

Na Mwanaisha Makumbuli
Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa Saba wa Kundi la Uendeshaji na Mkutano Mkuu wa Tatu wa Jukwaa la Ushirikiano la Mbegu na Bioteknolojia Afrika, unaolenga kuimarisha uratibu, ushirikiano na utekelezaji wa vipaumbele vya sekta ya mbegu barani humo.
Mkutano hiyo inayoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika, AUDA-NEPAD, kwa kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Afrika, AUC, inafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 10 hadi 13 mwaka 2026, ikiwakutanisha wawakilishi wa nchi za Afrika, taasisi za utafiti, mashirika ya wakulima, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
Lengo la mkutano hiyo ni kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora na vifaa vya kupandia, kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha usalama wa chakula na lishe pamoja na kujenga mifumo ya kilimo inayohimili mabadiliko ya tabianchi.
Katika mkutano hiyo, washiriki wanajadili pia namna ya kuboresha sera za mbegu, kuimarisha benki za mbegu na jeni, pamoja na kuendeleza mifumo ya mbegu inayosimamiwa na wakulima ili kuongeza ushiriki wao katika uzalishaji na uhifadhi wa mbegu.
Aidha, mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, watafiti, wakulima na sekta binafsi, huku ukipitia utekelezaji wa Mpango wa Mbegu na Bioteknolojia Afrika pamoja na kuweka mikakati ya utekelezaji kwa mwaka 2027 hadi 2028.
Matokeo yanayotarajiwa ni kuimarika kwa uratibu wa sekta ya mbegu, uwajibikaji, uwekezaji na upatikanaji wa mbegu bora, hatua zinazolenga kuongeza tija ya kilimo na kuchochea maendeleo endelevu pamoja na usalama wa chakula barani Afrika.