Highlands FM
Highlands FM
22 October 2026, 11:13 pm

Miili ya wanawake wawili yakutwa imefichwa uvunguni mwa kitanda jijini Mbeya. Polisi wafichua yaliyojiri katika uchunguzi wa tukio hilo la mauaji
Na Samwel Mpogole
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limemkamata mtuhumiwa Benson Steven maarufu kwa jina la Mkembo, akituhumiwa kuhusika na mauaji ya wanawake wawili ambao miili yao ilikutwa imefichwa uvunguni mwa kitanda katika nyumba ya kulala wageni ya Igogwe, eneo la Makunguru jijini Mbeya, Oktoba 16, 2026.
Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga amesema Uchunguzi wa awali ulidaiwa kubaini kuwa mtuhumiwa alihusisha tukio hilo na imani za kishirikina kwa lengo la kupata utajiri, huku mwili mmoja ukitambuliwa kuwa wa Annastazia Mwakipesile, mwenye umri wa miaka 32, na mwingine ukiendelea kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya kwa ajili ya utambuzi.
Hata hivyo, mtuhumiwa huyo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya baada ya kujeruhiwa kwa risasi katika paja la mguu wa kushoto, kufuatia jaribio la kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa polisi wakati akielekea kuwaonyesha askari nyumbani kwa mganga wa jadi anayedaiwa kuhusika na masharti hayo.