Highlands FM
Highlands FM
24 November 2026, 9:14 am

Mafuta kwenye madumu ni hatari kama bomu! EWURA yatoa onyo kali kwa wauzaji holela wa mafuta na kusisitiza usalama wa wananchi
Na Samwel Mpogole
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewaonya watu wanaojihusisha na uuzaji holela wa mafuta ya petroli na Diesel bila kuwa na leseni au vibali vinavyotakiwa, ikiwataka kutumia fursa za uwekezaji zilizopo, hususan katika maeneo ya vijijini ambako masharti ya uwekezaji yamepunguzwa.
Rai hiyo imetolewa na Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa EWURA, Walter Christopher, ambaye amesisitiza kuwa uuzaji wa mafuta kwenye madumu bila kufuata taratibu za kisheria ni hatari kwa usalama wa wananchi.
Aidha, Christopher ameonya kuhusu tabia ya baadhi ya vyombo vya usafiri kubeba mafuta kwenye vyombo vya plastiki, akieleza kuwa kitendo hicho ni hatari kubwa kinachoweza kusababisha madhara makubwa, akifananisha na mtu anayebeba bomu.
EWURA imewataka wananchi kuzingatia matumizi salama ya mafuta kwa kununua katika vituo vinavyotambulika, huku ikiwahimiza wawekezaji kuchangamkia fursa za kuanzisha vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.