Highlands FM

Bakwata yasisitiza amani na mshikamano Misikitini

4 October 2026, 11:23 pm

Kadhi wa Mbeya atoa ujumbe mzito kuhusu nafasi ya misikiti katika kujenga amani, upendo na mshikamano.

Na Samwel Mpogole

Waumini wa dini ya Kiislamu jijini Mbeya wametakiwa kutumia misikiti kama majukwaa ya kujenga upendo, mshikamano na amani katika jamii.

Wito huo umetolewa na Kadhi wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Mbarazi, wakati wa uzinduzi wa msikiti mpya eneo la Nsalaga jijini Mbeya. Sheikh Mbarazi amesema misikiti inapaswa kuwa sehemu ya kuwaunganisha waumini, kushauriana na kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali zinazowakabili katika jamii.

Sauti ya Kadhi wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Mbarazi

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa BAKWATA Mkoa wa Mbeya, Musa Abdala Ismail, amewapongeza wakazi wa Nsalaga kwa kukamilisha ujenzi wa msikiti huo, akiwataka kuutumia kuimarisha amani na umoja.

Amesema mshikamano wa waumini ni muhimu katika kuendeleza ibada na shughuli za maendeleo ya jamii.

Sauti ya Mwenyekiti wa BAKWATA Mkoa wa Mbeya, Musa Abdala Ismail

Waumini waliohudhuria uzinduzi huo wamesema kukamilika kwa msikiti huo kutarahisisha huduma za ibada na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wakazi wa Nsalaga.