Highlands FM

Wazee wataka mishahara ya vijana ikatwe kwa ajili ya kuwahudumia wazazi

9 November 2026, 8:47 pm

Baadhi ya wazee wakitembea kuelekea katika eneo la kukaa; Picha na Samwel Mpogole

Je, ni wakati sasa wa mishahara ya vijana kukatwa ili kuwahudumia wazazi? Wazee nchini wametoa pendekezo hilo wakitaka kurejesha heshima na wajibu wa watoto kwa wazazi wao

Na Samwel Mpogole

WAZEE nchini wameiomba Serikali kuweka sera na miongozo itakayowezesha sehemu ya mishahara ya vijana walioajiriwa kukatwa na kuelekezwa katika kuwahudumia wazazi wao, wakieleza kuwa baadhi ya vijana wamekuwa wakisahau wajibu wao kwa wazazi baada ya kupata ajira.

Mapendekezo hayo yametolewa wakati wa maadhimisho ya kileke cha Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Songwe, yakihudhuriwa na wazee kutoka mikoa mbalimbali nchini ambao wametoa maoni na mapendekezo mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha ustawi na huduma wanazopaswa kupata.

Sauti ya wazee, Tumikiwe Kabuki na
 Elieza Mrutu

Akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Abubakari Kunenge, amewataka watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali kutowatelekeza wala kuwahujumu wazee, bali kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya Serikali yanayolenga kuwalinda na kuboresha maisha yao, ikiwemo kuwakinga dhidi ya vitendo vya ukatili.

Sauti ya Abubakari  Kunenge – Mkuu wa Mkoa wa Songwe

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Amon Mpanju, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha huduma na mifumo ya ulinzi kwa wazee ili kuhakikisha wanapata haki na mahitaji yao ya msingi.

Sauti ya Amon Mpanju – Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii

Maadhimisho hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Zama za Maisha Marefu, Tuboreshe Huduma za Wazee.”

Baadhi ya wazee wakiwa katika maadhimisho; Picha na Samwel Mpogole