Highlands FM

Takukuru yashtukia upigaji fedha za kikundi Mbeya

9 November 2023, 12:39

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Mbeya Maghela Ndimbo : Picha na Samweli Mpogole

Mwandishi Samweli Mpogole

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani Mbeya imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi milioni 50, fedha za kikundi cha Isongole Bambo, wilayani Rungwe ambazo ni mkopo uliotolewa na halmashauri kwa ajili ya kuyawezesha makundi ya wanawake, vijana na makundi maalum.

Mkuu wa taasisi hiyo mkoa wa Mbeya Maghela Ndimbo amewaeleza hayo waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi yenye thamani ya zaidi ya sh.bilioni 37. Kwa mujibu wa Ndimbo kikundi hicho kilianza shughuli zake mwaka 2001na kilisajiliwa mwaka 2017 chini ya halmashauri hiyo na kisha kupewa mkopo huo Disemba 2021 ili kufikia malengo yao.

Ndimbo ameongeza kuwa baada ya kupewa mkopo huo kikundi hakikufanyia kazi fedha hizo kama walivyoomba mkopo badala yake waligawana na kukubaliana kuzirejesha jambo ambalo baadaye liliwaletea ugumu na kushindwa kurejesha.

Mpaka sasa Takukuru imeingilia kati kwa kukaa kikao na wanakikundi hao ambapo wamefanikiwa kurejesha Tsh 11,860,000 kati ya milioni 43 ambazo wanadaiwa wanakikundi hao.

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mbeya Maghela Ndimbo